# Je, Ni Kosa kwa Mwanaume Kuoa Mwanamke Mwenye Watoto wa Baba Wengine?
Katika jamii zetu, zamani ilikuwa sio kitu Cha kawaida kwa mwanaume kuoa na kuishi na mwanamke mwenye watoto aliozaa na mwanaume mwingine, kwa baadhi jamii ilionekana kama kuleta au kumkaribisha watu wa nje kwenye jamii. Lakini kipindi hicho mambo yalikuwa tofauti na sasa. Hata kumpata mwanamke wa jinsi hiyo kwenye jamii ilikuwa kitu nadra sana.
Mabinti walijitunza na kujiheshimu Kutoshiriki kuzaa kabla ya Ndoa. Mabinti hawakuozwa kabla ya kufundwa na kungwi ayewapatia mafunzo ya maisha. Katika miaka ya hivi karibuni hali imebadilika baada ya Dunia kupotoka na kukiuka maadili. Siku kumpata mwanamke wa kuoa ambaye hajazaa inaweza kuwa kibarua fulani. Hata hivo suala la mwanaume kuoa mwanamke mwenye watoto kutoka mahusiano ya awali limekuwa likijadiliwa kwa mitazamo tofauti.
Kuna baadhi ya Wanaume wasiopenda kuoa mwanamke mwenye watoto wa kufikia na Kuna wale wasiopenda. Wapo wanaoamini kuwa upendo wa kweli hauchagui historia ya mtu, huku wengine wakiona changamoto zinazoweza kujitokeza katika malezi na ujenzi wa familia mpya. Moja ya sababu zinazotajwa mara kwa mara kuvuruga mahusiano ya aina hii ni tofauti za mtazamo kuhusu malezi na nidhamu ya watoto.
#Mwanaume Anapoingia Kwenye Wajibu wa Ulezi wa Mwanaume Mwingine,
Mara nyingi mwanaume anayemwoa mwanamke mwenye watoto huingia katika maisha ya familia hiyo kwa nia njema. Anajitahidi kuwapa watoto chakula, mavazi, ada za shule, matibabu na mahitaji mengine muhimu. Kadiri muda unavyopita, huanza kujiona kama mlezi na mzazi anayewajibika katika familia hiyo.
#Lakini changamoto huanza pale ambapo suala la nidhamu linapojitokeza.
Watoto wanapokosea na mwanaume akaamua kuwaadhibu au kuwaonya kwa lengo la kuwajenga kitabia, baadhi ya wanawake hukasirika na kuona kana kwamba watoto wao wananyanyaswa. Katika hali kama hizo, mwanaume anaweza kusikia maneno makali kama:
"Usinipigie mwanangu!"au
"Unawachapa watoto kwa sababu hukuwazaa!".na mara nyingine,
Wengine hufikia hatua ya kusema:
"Unawapiga hao watoto, unajua nilipowatoa?"
Kauli kama hizi humkatisha tamaa na kumuumiza mwanaume ambaye amekuwa akijitolea kwa moyo wake wote kuhakikisha familia hiyo inaishi kwa amani na ustawi, japo kutokana na kauli za mkewe matatizo ya kutoelewana huanzia hapo. Wanawake wa jinsi hii humtaka mwanaume aliyemwoa awe mtumwa wa familia hiyo ila asithubutu kuwagusa watoto ambao sasa huwaita wake japo kawakabidhi mume huyo.
# Athari za Maneno jayo Kwenye Mahusiano
Tatizo kubwa siyo tu suala la adhabu, bali namna ambavyo migogoro hiyo hushughulikiwa. Mwanaume anapohisi juhudi zake hazithaminiwi na mamlaka yake ndani ya nyumba yanapingwa kila mara, huanza kupoteza hamasa ya kuwajibika kama mzazi wa wanawe.
Hasira zinapoongezeka, naye anaweza kujibu kwa maneno makali kama:
"Ni kweli sijui ulipowatoa, basi nenda uwarudishe kwa baba yao."
Kauli kama hizi huongeza ufa uliokuwepo kwenye mahusiano. Badala ya kutatua tatizo, hujenga chuki, majeraha ya kihisia na kutokuaminiana. Mwishowe, ndoa au mahusiano huvunjika.
# Mzunguko Unaoweza Kujirudia
Baada ya kuachana mwanamke anaweza kujikuta akirejea katika maisha ya kuwa mzazi pekee. Wakati mwingine huingia kwenye mahusiano mengine akiwa bado na watoto wake. Endapo mwanamke kama huyu hawezi kubadili tabia yake kutoa fursa ya malezi shirikishi au mawasiliano na mipaka ya uwajibikaji, migogoro kama hiyo inaweza kujirudia tena na mwisho wa siku ataishia kuhesabu Wanaume.
Katika baadhi ya matukio, mwanamke anaweza kupata mtoto mwingine katika mahusiano mapya kabla hata ya mahusiano hayo kuwa imara. Hali hiyo inaweza kusababisha familia kuwa na watoto wenye baba tofauti, jambo ambalo huongeza changamoto za malezi, uwajibikaji na uthabiti wa familia.
# Je, Hili Ndilo Chanzo au Tatizo Pekee?
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa si sahihi kusema kwamba sababu hii ndiyo chanzo pekee cha wanawake kuwa na watoto wasiokuwa wa baba mmoja. Sababu za kuvunjika kwa mahusiano ni nyingi, zikiwemo ukosefu wa mawasiliano, ukatili wa familia, kutowajibika kwa baadhi ya wazazi, matatizo ya kiuchumi, usaliti na tofauti za kimaadili. Kuna malalamiko ya akina dada wengi ambapo baadhi ya Wanaume wamewatesa hata watoto wao wa kuzaa wenyewe. Mwanaume kama huyo hawezi kuleta watoto wa kufikia. Baadhi pia huwalaghai wadada kuwapenda watoto wao na kisha kubadilika baadaye.
Lakini jambo moja lipo wazi:
Pale ambapo mzazi mmoja anataka mtoto apewe nidhamu na mwingine anapinga kila hatua ya malezi, migogoro huwa karibu kutokea. Familia inahitaji makubaliano ya pamoja kuhusu namna ya kulea watoto ili kuepuka migawanyiko inayoweza kuharibu mahusiano.
# Hitimisho
Kuoa au kuolewa ukiwa na watoto kutoka mahusiano ya awali si tatizo lenyewe. Changamoto kubwa ni namna wahusika wanavyojenga mawasiliano, kuheshimiana na kuweka misingi ya malezi inayokubalika kwa wote. Bila kufanya hivyo, migogoro inaweza kuongezeka na kuathiri si tu wanandoa bali pia watoto wanaohusika.
**Swali la kujiuliza ni hili: Je, ni kisa kwa mwanaume kuona mwanamke mwenye watoto wa baba wengine, au changamoto halisi ipo kwenye namna familia hizo zinavyojengwa na kuendeshwa baada ya kuungana?**
