#KENYA KATIKA G7: HESHIMA YA VIWANGO AU KUIGA KUNYA KWA TEMBO?

 #G7 ni Nini na ni Nchi Zipi?

G7 yaani *Group of Seven*  ni muungano usio rasmi wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa zaidi duniani ya nchi zilizoendelea kiviwanda. Nchi hizo ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani, pamoja na Umoja wa Ulaya ambao nao hushiriki.

Mkutano wao si tu wa kiprotokali. Ni jukwaa ambalo maamuzi yanayoathiri mabilioni ya watu duniani yanazaliwa  kuhusu uchumi, usalama, hali ya hewa, teknolojia na fedha za maendeleo.

Mkutano wa  mwaka 2026 unafanyika Évian-les-Bains, Ufaransa, kuanzia Juni 15 hadi 17, chini ya urais wa Ufaransa katika G7, na unatarajiwa kushughulikia utulivu wa uchumi wa dunia, usalama, mabadiliko ya hali ya hewa, teknolojia na ufadhili wa maendeleo. 

# Kwa Nini Kenya Ilihudhuria? Kenya Haikuomba ila Iliombwa kuhudhiria mkutano huo. Hii ndiyo sehemu muhimu ambayo wengi wanaipuuza. Kenya haikujiingiza kwenye swala hili G7. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimwomba Rais William Ruto ahudhirie ili maoni ya Afrika kuhusu mageuzi ya mfumo wa fedha duniani na maendeleo yenye usawa yashirikishwe moja kwa moja katika ajenda ya G7.

Mwaliko huo ulipokelewa rasmi wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa Paris kati ya Balozi wa Kenya na Ufaransa Betty Cherwon na Katibu Mkuu wa Mipango ya Uchumi Boniface Makokha, wakati nchi ilikuwa inajitayarisha kwa Mkutano wa Mawaziri wa Maendeleo wa G7.

Kenya ilishiriki mkutano huo pamoja na nchi nyingine zilizoombwa kama Korea, Brazil na India kama ishara ya kupanda kwake katika kundi teule la uchumi zinazoibuka zinazoshirikishwa katika mazungumzo ya ngazi ya juu na mataifa makubwa zaidi duniani. 

# Je, Ruto Anawakilisha Kenya au Afrika?

 Jibu la swali hili liko katika  pande mbili na hii ndiyo changamoto ya kweli.

Rais Ruto alisema waziwazi wakati wa ibada ya kanisa Kajiado mnamo Juni 14, 2026, kwamba atasafiri Ufaransa kuwakilisha bara la Afrika katika mkutano huo wa G7.

Lakini hapa ndipo swali zito linaingia: Je, ametumwa na nani kuiwakilisha Afrika?  Hakuna rekodi ya mkutano wowote wa Umoja wa Afrika (AU) ulioamua Kenya iwe mwakilishi rasmi wa Afrika. Kenya ndiyo nchi pekee ya Afrika iliyoombwa kuhudhuria mkutano huo wa Viongozi wa G7 mwaka 2026. Kwa mantiki hiyo Rais William Ruto alipaswa kwenda kwenye mkutano huo kwa ajili ya Nchi yake, Kenya.

Ingawa Kenya imeshiriki katika mikutano mitatu ya G7 tangu 2017, ushiriki wake mwaka huu umevutia umakini zaidi, hasa baada ya Afrika Kusini kuripotiwa kutengwa kufuatia shinikizo la Marekani. 

Kwa hivyo Ruto anabeba "agizo" lake mwenyewe kwa heshima, lakini bila kura za Afrika. Kwa Uchambuzi wa kina, hatua hii ya mwaliko kwenye mkutano wa G7 wa mwaka 2026 unafuatia uswahiba wake na Rais Emma Macron wa Ufaransa na Donald Trump wa Marekani. Hawa ni watu wenye lengo la kupenyeza sera zao kwa Afrika kupitia Kenya.

# Uchumi wa Kenya Dhidi ya G7: Tofauti ya Anga na Ardhi

Hapa ndipo penye ukweli halisi unavyobana. Hebu tuangalie takwimu:

*Pato la Taifa (GDP) la Kenya ni dola bilioni 147 kwa kwa viwango vya mwaka 2026, ikiifanya iwe nchi ya 62 kwa ukubwa wa uchumi duniani.

*GDP kwa kila mtu wa Kenya ni dola 2,714 tu mwaka 2026.

Kwa ulinganisho na Nchi za G7: 

*GDP ya Marekani peke yake inazidi dola trilioni 27. GDP ya Japan ni trilioni 4. Hata Italia ndogo kabisa ya G7 ina GDP karibu trilioni 2. Kenya ni kama chembe ya mchanga katika bahari ya uchumi wa G7.

Zaidi ya hayo, asilimia 41.9 ya Wakenya wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa kimataifa wa dola 3 kwa siku  na ajira rasmi ni asilimia 15 tu ya nguvu kazi.

Kenya pia inakabiliwa na hatari kubwa ya msongo wa deni la Taifa linalokimbilia Trilioni 14, na uimarishaji wa bajeti bado ni changamoto kubwa huku Serikali ya Rais William Ruto ikikabiliwa na tuhuma za rushwa na ufisadi karibu katika kila idara na vitengo vya Serikali. Rais Ruto amekuwa akibaliwa na shinikizo la kupunguza ukopaji usio na tija na Kupinga bajeti ya Ikulu.

Uchambuzi wetu unalichukulia swala la mwaliko wa Kenya kwenye mkutano wa G7 kama Unafiki wa kiuchumi au vinginevyo Rais Ruto atakuwa anatumika kama chambo kwa mataifa ya magharibi kufikia baadhi ya malengo Yao kwa Afrika.

# Kenya Itanufaika Nini? Matarajio Halisi

Licha ya tofauti kubwa za uchumi, ushirikiano wa Kenya na mataifa hayo unaweza kuwa na manufaa kama:

1. Madeni na Muundo wa Fedha:

Moja ya mada muhimu ambayo Ruto anaweza kuitumia ni mazungumzo ya kurekebisha madeni. Karibu nusu ya bajeti ya Kenya inaenda kulipa madeni, kwa hivyo mazungumzo yenye tija yanaweza kuwa ombi kwa washirika wa G7 kuhusu jinsi ya kurekebishiwa au kuondolewa kwa madeni ya Kenya.

2. Ufadhili wa fedha za Mabadiliko ya Tabia Nchi:

Kenya imejiwekea msimamo wa kutetea ufadhili wa hali ya hewa, ustawi wa uchumi shirikishi, na mageuzi ya taasisi za fedha za kimataifa. 

3. Uwekezaji na Teknolojia:

Mkutano wa G7 unatoa fursa kwa Kenya kujiweka kama lango la Afrika kwa uwekezaji, uvumbuzi, na ushirikiano wa kimataifa. 

4. Nguvu ya Kidiplomasia;

Mwaliko huu unaonyesha kuongezeka kwa uonekano wa kidiplomasia wa Kenya na jukumu lake linaloongezeka kama moja ya sauti zenye ushawishi wa Afrika katika masuala ya kimataifa.

# Hoja kuu kwa Kenya: Je, ni "Kuiga Kunya kwa Tembo"?

Hoja ya "kuiga kunya kwa tembo" ina msingi wa kweli unaostahili kuchukuliwa kwa uzito.

*Mosi: 

Kenya si mwanachama wa G7* na haitakuwa hivi karibuni kutokana na viwango vyake kuwa chini, katika swala hili inaonekana  kuingia chumba ambacho haikijemgi na ambacho maamuzi yake ya msingi yanafanywa bila ridhaa Wala ushiriki wake!?

*Pili: 

Hakuna kura za Afrika.* Ruto anasema anawakilisha Afrika, lakini hakuna mkutano wa Afrika uliomtuma. Hii inamaanisha sauti yake, hata nzuri kiasi gani, ni sauti yake mwenyewe si ya mabunge au wakuu wa AU waliokaa pamoja na kuamua.

*Tatu: 

Tatizo la uhalali wa ndani. Safari ya Ufaransa inakuja wakati ambapo serikali inakabiliwa na ukosoaji mkali wa ndani kuhusu safari nyingi za nje za Ruto, na maswali kuhusu manufaa yanatotokana na gharama ya safari hizi za diplomasia.

Udadisi wetu unaziona safari za nje za Rais Ruto kama zenye gharama kubwa isiyofidiwa na matokeo yanye tija, hasa pale inapodhihirika kutoakisi mabadiliko kwa mwanachi wa kawaida.

Lakini je, hoja hii inaisha hapo? Hapana.

Wachambuzi wa mahusiano ya kimataifa wanasema Afrika inatafuta sauti kubwa zaidi katika utawala wa kimataifa na sehemu ya haki ya fursa zinazopatikana katika dunia inayounganika zaidi. Bila kukaa mezani, utabaki ukiliwa bila ridhaa yako.

Ruto ataona mwaliko huu kama uthibitisho wa juhudi zake za kuwasilisha Kenya kama mpatanishi wa kutegemewa kati ya nguvu za kimataifa. 

Swali la msingi basi ni hili: Je, ni vema kuhudhuria kwa hofu ya kukosekana (mfumo rasmi wa kidiplomasia) au ni busara kufanya hivi kwa unyenyekevu unaojifanya nguvu?

# Hitimisho: Hatua ya Busara au Uigaji wa Heshima?

Ukweli uko katikati ya hoja mbili. Kenya haina nguvu za kiuchumi za G7,  hiyo ni ukweli mgumu. Lakini diplomasia ya kimataifa haifanyi kazi kwa GDP peke yake. Inafanya kazi kwa ushawishi, uhusiano, na uwezo wa kuweka ajenda.

Fursa kama hizi huwa haziji kwa kujirudia. Mataifa yanayoelewa hili yanashika mkono wa fursa kwa nguvu zote mbili. Kenya sasa imesimama mbele ya wakati kama huo. Kama itauendea kwa mkakati na makusudio, mkutano wa G7 wa 2026 unaweza kuwa hatua ya mabadiliko katika safari ya nchi hiyo kuelekea ustawi mkubwa zaidi, ushawishi na umuhimu wa kimataifa.

Tatizo hapa si kuhudhuria. Tatizo ni kurudi nyumbani mkono tupu*bila mikataba ya madeni, bila fedha za miradi ya hali ya hewa na mabadiliko ya Tabia nchi, bila uwekezaji wa kweli. Kama hivyo ndivyo itakavyotokea, basi ndiyo "kuiga kunya kwa tembo"

Jicho la Afrika kwa Kenya litakuwa kwenye matokeo na si kwenye picha tu.

Post a Comment

Previous Post Next Post