#KWANINI KENYA IMEINGIZWA MTEGONI KITUO CHA EBOLA?

 Serikali ya Kenya imeingia kwenye mtego wa kuiridhia Serikali ya Marekani kujenga/ kuanzisha kituo cha karantini na matibabu ya Ebola nchini humo bila kushirikishwa Umma. 

Kituo hicho kilichoanzishwa kwenye Kambi ya Kijeshi ya Laikipia nchini humo  kinaandaliwa kwa Ajili ya kuwahudimia/kuwatibu Wamarekani walio katika hatari ya kuambukizwa Ebola au kuugua ugonjwa huo wakati wa mlipuko unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda. 

1. SABABU KUU:

 Lengo la kituo hiki ni kuwaleta wamarekani wanaougua Ebola kutoka DRC kuja Kenya

Mpango wa serikali ya Marekani ni kuwahamishia nchini Kenya raia wake waliopo katika hatari kubwa ya maambukizi (lakini bado hawajaanza kuonesha dalili) kwa ajili ya uangalizi wa karibu. Hata hivyo, kulingana na mabadiliko ya mpango huo, Wamarekani watakaogundulika kuwa na dalili kali au kuugua watatibiwa nchini Kenya, badala  ya kuwasafirisha moja kwa moja hadi Marekani.

2. KWANINI IWE KENYA?

I) Kuwasaidia Raia wa Marekani: Lengo kuu lilikuwa kuweka karantini na kuwatibu wataalamu au raia wa Marekani watakaokutana na maambukizi katika eneo la maziwa makuu. 

ii) Ukaribu wa Kijiografia: Kenya iko karibu na DRC, hivyo kituo hiki kilionekana kuwa njia ya haraka ya kupata matibabu badala ya kuwasafirisha wagonjwa hadi Marekani au Ulaya. 

iii) Ushirikiano wa Kidiplomasia: Hatua hiyo ilionekana kama muendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu wa kimkakati kati ya serikali hizo mbili kwenye masuala ya afya ya umma. 

iv) Kudhibiti Mlipuko: Serikali ya Kenya ilitafuta njia za kujiweka tayari na kupokea misaada ya vifaa vya kitabibu na utaalamu kutoka Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Marekani (HHS).

3. SABABU ZA KUPINGWA:

I) Ukiukwaji wa Sheria na Haki za Kikatiba: 

Taasisi ya Katiba (Katiba Institute) ilidai kuwa uamuzi huo ulichukuliwa kwa siri bila kuwashirikisha wananchi na ulikiuka utaratibu wa Bunge la Kenya.

ii) Ukosefu wa Miundombinu:

 Wataalamu wa afya walisema Kenya haina maabara za kisasa zaidi (Biosafety Level 4) zinazohitajika kudhibiti magonjwa hatari kama Ebola

iii) Ubaguzi na Hofu ya Maambukizi: Wananchi na vyama vya madaktari walihoji kwanini kituo hicho kitengwe kwa ajili ya Wamarekani pekee na kuonesha hofu ya kuingiza kirusi hicho kwenye nchi ambayo haikuwa na kisa kilichothibitishwa. 

iv) Hofu ya Usalama wa Takwimu: Kulikuwa na wasiwasi kuwa makubaliano hayo yangeweza kutoa mwanya kwa Marekani kudhibiti taarifa nyeti za kiafya za kiafrika.

4. Kwa nini kituo hiki kisiwekwe DRC ambako ndiko ugonjwa ulipoanzia?

Maafisa wa afya wanaeleza kuwa DRC inakabiliwa na uhaba mkubwa wa usalama, mapigano ya wanamgambo, na uhasama wa jamii dhidi ya vituo vya afya, hali inayoweka maisha ya wagonjwa na madaktari hatarini. Eneo la Ituri na Kivu Kaskazini linakabiliwa na machafuko ya mara kwa mara, ambapo wananchi wamekuwa wakivamia na kuchoma moto vituo vya matibabu kwa madai ya kutokubaliana na itifaki za ugonjwa huo. Hivyo, Marekani imeona ni hatari sana kusimamia kituo cha matibabu ya kibiolojia (biocontainment ward) kwenye mazingira hayo yasiyo na utulivu.

5. Sehemu iliyopendekeza/ Kuamriwa:

Kituo hicho kilichoidhinishwa kuwa na vitanda 50 kilitarajiwa kujengwa ndani ya kambi ya kijeshi ya Laikipia Air Base, ingawa serikali na Wizara ya Afya ilipanga pia kutumia maabara za KEMRI na Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma kwa ajili ya uchunguzi.

6. PINGAMIZI LA KISHERIA:

Taasisi ya utetezi wa sheria na haki za binadamu ya Katiba Institute imefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi kupinga mpango huo wa siri kati ya serikali ya Kenya na Marekani. Katiba Institute imeomba mahakama izuie serikali ya Kenya kuruhusu ujenzi wa kituo hicho na kuingizwa kwa wageni kutoka maeneo yenye maambukizi ya Ebola. 

ÀGIZO LA MAHAKAMA:

Kutokana na hatua hiyo Mahakama ya Kenya (Milimani) imesimamisha kwa muda kuanzishwa/ Kuendeshwa/ kuhusika kwa namna yoyote shughuli za kituo hicho Cha Ebola hadi shauri hilo litakapoamriwa.

7.) MGOMO NA MAANDAMANO:

 Jambo hili tayari limezua taharuki na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi wa kawaida na wataalamu wa afya. Muungano wa Madaktari na Wauguzi nchini Kenya (KMPDU) umetoa notisi ya saa 48 kwa serikali kufichua wazi mkataba huo wa karantini, na umetishia kuanzisha mgomo mkubwa wa kitaifa iwapo serikali itashindwa kutoa maelezo ya kutosha na kuweka maslahi ya wakenya mbele. Hata hivyo uwezekano wa mgomo halali ni pale Serikali itakapokaidi Agizo la mahakama.

Post a Comment

Previous Post Next Post