#DHIFA YA KITAIFA YA MAOMBI YA MARIDHIANO

 Tukio la Mei 28, 2026, la dhifa ya Kitaifa ya maombi ya Maridhiano ambapo wabunge wa Seneti na Bunge la kitaifa pamoja na Viongozi wa Serikali

walishiriki kiamsha kinywa pamoja katika Hoteli ya Safari Park, Jijini Nairobi ni moja ya Matukio makubwa ya kinafiki na ufujaji wa fedha za walipa kodi.

Hii ni kwa Sababu ya tukio lile kukosa maana Halisi ya Maridhiano au Upatanisho hasa kwa kushirikisha pande zote zinazohusika katika vita ya kauli na matamshi ya viongozi wa Kisiasa zinazohatarisha umoja na amani ya nchi zilizoshuhudiwa hivi karibuni.

 Kwa maoni yetu, tudhani tukio la kushiriki kiamsha kinywa na maombi ya Kitaifa halipaswi kuwa swala na kula na kunywa na kualika kwaya za nyimbo za injili, bali ushiriki halisia wa viongozi wote wa Kisiasa wanaotoa matamshi na kauli za uchochezi.

Upatanisho (reconciliation) humaanisha kurejesha uhusiano mzuri, kusuluhisha tofauti, na kusameheana makosa ya nyuma. Matarajio ya wengi Katika muktadha huu wa Maombi ya Kitaifa  yaliyofanyika katika Hoteli ya Safari Park, ilikuwa ni wito wa kuleta uponyaji wa kisiasa, umoja, na kuweka kando migawanyiko ya kisiasa na kikabila.hasa katika kipindi hiki ambapo taifa linaelekea kwenye Uchaguzi wa mwaka ujao wa 2027.

Wahusika Wakuu wa Maridhiano:

 Kimsingi, pande zilizotakiwa kuwepo kwenye Maridhiano ya aina hii ni pamoja na viongozi wa kisiasa kutoka kambi pinzani hususan Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Martha Karua, Fred Matiang'i, Edwin Sifuna, Babu Owino miongoni mwa wengine (muungano wa serikali na upinzani Broadbased), pamoja na viongozi wa serikali walio na mizozo ya ndani kwa ndani, mathalani mzozo wa kauli na matamshi ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar yaliyozua hofu na uchochezi kwa jamii, kauli za Wabunge wa eneo la mlima Kenya dhidi ya matamshi ya Hassan Omar, haya ndio mambo muhimu ambayo yalitakiwa kupewa vipaumbele ili kupunguza joto la kisiasa linalozidi kupanda. 

Kamwe hili sio swala la vigogo kwenda kukaa kwenye Hoteli kubwa kula na kunywa kushuhudia kwaya zikiimba, Nyimbo za kwaya zimekuwepo siku zote hata majumbani mwa watu zinasikilizwa na kuangaliwa. Muhimu ni kauli za viongozi kukiri na kuwa na Upatanisho wa wazi.

Je, hii Ilikuwa ya Sadifa? (Irony)?

 Tunalichukulia tukio hili kama Unafiki na Sadifa. Kwa sababu kinachohubiriwa sio kinachotendeka isipokuwa kinyume chake. Hii ni kwa sababu viongozi hao wanatumia jukwaa la kidini tena kwa ufadhili wa fedha za Umma, kuhubiri amani na msamaha tena bila ushiriki  wa walengwa wote muhimu, lakini wanapotoka tu ukumbini, wanaendelea na siasa za matusi, uchochezi, na utengano.

Kuhudhuria Viongozi wa Upinzani:

 Kuna madai kwamba viongozi wa upinzani wakati mwingine hususia au kutohudhuria tukio hili. Mara nyingi huwa hawaalikwi au hawajitokezi kwa sababu wanaona ni kama jukwaa la kujipigia debe kisiasa linalotumiwa na viongozi wa serikali kufunika masuala nyeti ya nchi badala ya kufanya mazungumzo ya kweli. Kwa vile wao ndo walengwa wakubwa wa Maridhiano ya aina hii, Kutoshiriki kwao ni moja ya vigezo vinavyohalalisha kufutwa kwa dhifa hiyo kutoka kwenye kalenda ya Taifa kwa Sababu waanzilishi wa shughuli hiyo hawakuzingatia athari za milengo ya Kisiasa.

Waandaaji wa Hafla Hii: 

Hii ni ishara tosha Kwamba Mabunge yote ya Kenya ambayo ndo wandaaji wa dhifa hiyo, yanashiriki katika kufuja pesa za Umma kwa Hafla na dhifa zisizokuwa na tija. Hafla hii huandaliwa na Bunge la Kenya. Inaendeshwa kwa mfumo wa mzunguko ambapo mara nyingi huandaliwa na Bunge la Seneti kwa kushirikiana la Bunge la Kitaifa.

Matumizi Mabaya ya Kodi za Wananchi:

 Wananchi wengi wana mtazamo kwamba kutumia mamilioni ya fedha za umma kwa ajili ya kiamsha kinywa katika hoteli za gharama ni matumizi mabaya ya kodi zao. Hii inaleta utata mkubwa hasa wakati wananchi wa kawaida wanapitia changamoto kubwa za kiuchumi huku Serikali ya Rais William Ruto ikishindwa hata kuwapunguzia Bei ya Mafuta. Zipo taarifa kwamba hata mahakama zimewahi kuitaka Bunge kuweka wazi bajeti ya matumizi ya hafla kama hizi.

Kama kama Kuna haja ya kufanyika tukio la jinsi hii, ni kwanini lisifanyike kwenye Viwanja vya wazi ambapo Wananchi wote wanaweza kushiriki maombi na Viongozi wanaohasimiana au wenye migogoro wakaongea hadharani ili wananchi wawashuhudie kwa kauli zao kwamba Kuna makubaliano ya Maridhiano? Si lazima watu wale na kunywa vyakula vya gharama, tunadhani jambo kubwa hapa ni amani na mshikamano inayopatikana.

Hatua ya shughuli hii kufanyika mafichoni kwenye Hoteli za kifahari ni zenye lengo la kifisadi kwenye matumizi ya pesa hasa kwenye posho za Wabunge na Wageni waalikwa, bili kubwa za vyakula na vinywaji na gharama za mafuta ya Magari. Inasikitisha kwamba Rais wa nchi anaweza kuingizwa mkenge kushiriki mambo kama haya.

Hafla/Dhifa hii Iondolewe:

Ni maoni yetu Kwamba kifutwe kipengere Cha Sheria ya Bunge au Katiba kinachoruhusu kufanyika kwa  sherehe hii na zinginezo zinazofanana nayo ili fedha hiyo ihamishiwe kwenye maeneo mengine yenye uhitaji. Hata hivyo, tunaamini kwamba imepoteza thamani yake ya awali kwani maombi hayo hayabadili utamaduni mbaya wa kisiasa wala kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.  

Wanasema ukiiga kunya kwa tembo utapasuka msamba, ndivyo ilivyo kwa utamaduni huu ulioigwa kutoka Marekani ambao hauna faida kwa wakenya, Kama waliiga katiba, wakaiga uwepo wa Mabunge mawili, Bunge la Seneti la Kitaifa, Bado hiyo haikutosha wakaiga tena sherehe kama hizi zenye lugha ya maombi ya kuridhiana ambapo hata wanatakiwa kuridhiana hawahudhurii. Wakenya wanaopaswa kuelewa kwamba sio kila kitu kinachoigwa kina faida.

Toa maoni yako....


Post a Comment

Previous Post Next Post