#Katika mahojiano na Jeff Koinange kwenye Kipindi Cha JKL kinachorushwa na Citizen Tv, Methu alisema matamshi yake aliyoyatoa tarehe 8 Aprili wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Nyandarua, marehemu David Keraho hayakiwa dharau au dhihaka kwa Rais. Kauli hiyo ya Methu ilizua mjadala mkali kisiasa na mitandaoni, huku baadhi wakidai kuwa alimkosea heshima Rais William Ruto.
#“Sikumdharau Rais” – Methu Ajitetea
Akizungumza kwenye kipindi hicho, Seneta Methu alisisitiza kuwa hakukuwa na nia ya kumdharau wala kumdhihaki Rais aliposema kuwa anamheshimu kama Rais na Amili Jeshi Mkuu ila, “hamuogopi.” Badala yake, alieleza kuwa kauli yake ilikuwa njia ya kufikisha ujumbe muhimu kwa Rais kuhusu hali halisi inayowakumba wananchi wa Nyandarua
Kwa mujibu wake, kauli hiyo ilitokana na kutoridhishwa na utekelezaji wa baadhi ya ahadi zilizotolewa na Rais kwa Wananchi wa eneo analoliwakilisha.
# Fursa Adimu ya Kumfikia Rais
Methu alieleza kuwa siku ile alipata fursa ya kipekee kwa sababu si rahisi kwa viongozi kama yeye kukutana na Rais mara kwa mara kama ilivyo kwa Gavana au Mbunge.
Alisema kuwa uwepo wa Rais katika eneo lake ulimpa nafasi ya moja kwa moja kuwasilisha kilio cha wananchi wake, jambo aliloona ni wajibu wake kama kiongozi.
# Kutoka Mshirika Hadi Mkosoaji
Katika maelezo yake, Seneta huyo alifichua kuwa hapo awali alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Rais Ruto na hata alishiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi uliopita kwa kumuunga mkono na kumpigia debe.
Hata hivyo, kwa sasa amesema ameghairi uungwaji mkono wake kutokana na kile anachodai kuwa ni kushindwa kwa Rais kutekeleza ahadi zake. Aidha, ameweka wazi kuwa anaunga mkono mjadala wa “muhula mmoja” (One Term) kwa Rais, akisisitiza kuwa uwajibikaji lazima uwepo kwa viongozi wakuu.
#“Nililazimika Kusema Hadharani”
Methu alisisitiza kuwa sababu kuu ya kusema hadharani ni kwa kuwa masuala aliyoyazungumzia yanawahusu moja kwa moja wananchi wa Nyandarua. Kwa mtazamo wake, uwazi na uwajibikaji vinahitaji viongozi kusema wazi wanapohisi wananchi wao hawapati haki wanayostahili.
#Matokeo Yameanza Kuonekana?
Katika hoja ya kuvutia zaidi, Seneta huyo alidai kuwa kauli yake tayari imeanza kuzaa matunda. Alisema kuwa baada ya tukio hilo, wakandarasi walitumwa kufanya tathmini ya moja ya barabara katika kaunti ya Nyandarua pamoja na uwanja wa michezo—miradi ambayo hapo awali ilikuwa haijapatiwa kipaumbele.
Kuasi chama
Je matamshi na kauli za John Methu yanamaanisha kukiasi Chama Cha UDA kilichombeba kwenye uchagizi iliyopita? Yeye binafsi anakiri kubadilisha mkondo wa kisiasa na alipoulizwa endapo hatakuwa kigeugeu kwa leo kusema hivi na kesho akarejea tena, John Methu alisema ameshapima upepo na ametembea maeneo mengi ya Kenya na kuona kwamba 'Ground ' Wananchi wasema ni Muhula mmoja kwa Raia Ruto.
#Hitimisho
Kauli ya Seneta John Methu imeibua mjadala mpana kuhusu mipaka ya uhuru wa lugha kwenye majukwaa ya kisiasa, heshima kwa mamlaka ya juu, na wajibu wa viongozi kwa wananchi wao. Je, ilikuwa ni hatua ya ujasiri ya kuwatetea wananchi au ni siasa za kujipambanua?
Jambo lililo wazi ni kuwa sauti yake imeongeza presha kwa serikali kuu kuangalia kwa karibu maendeleo ya Nyandarua—na huenda hii ikawa mwanzo wa mjadala mpana zaidi kuhusu uwajibikaji wa viongozi nchini.
