Katibu Mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyazi nchini Kenya, Francis Atwoli amenukuliwa
mara kadhaa alisema kwa ujasiri kwamba hakuna UPINZANI Kenya. Sasa kabla ya kujadili hoja hii hebu kwanza tumwangalie Francis Atwoli ni nani?Francis Atwoli ni nani?
Francis Atwoli ni kiongozi mkongwe wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya ambaye amehudumu kama Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (COTU-K) tangu Agosti 2001. Yeye ni mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa zaidi katika masuala ya wafanyakazi, akishikilia nyadhifa za uongozi katika ngazi ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Upekuzi wetu unaonyesha hadi Kufikia Machi 14, 2026, Francis Atwoli alichaguliwa tena bila kupingwa kwa muhula wa sita mfululizo kama Katibu Mkuu wa COTU-K katika mkutano wa wajumbe wa Baraza la Uongozi huko Kisumu. Uongozi huu unamwongezea muda hadi 2031.
Mambo yaliyochangia ushindi wake:
1. Hakuwa na mpinzani mwenye ushawishi miongoni mwa vyama vya wafanyazi zaidi yake. Atwoli aliungwa mkono na vyama 42 vya wafanyakazi, akionyesha kuungwa mkono kwa pamoja na kukosekana kwa upinzani wenye nguvu ndani ya muundo wa chama.
2. Uzoefu na Ushawishi: Wafuasi wake wanataja uzoefu wake usio na kifani na uwezo wake wa kuwakilisha wafanyakazi katika ngazi za juu za serikali na majukwaa ya kimataifa.
3. Utulivu wa Kazi: Wajumbe walisifu utulivu aliouleta katika vuguvugu la wafanyakazi kwa miaka yake 25+ ofisini.
4. Kuungwa mkono na kikubalika Serikali
Mwelekeo wake wa kisiasa
Atwoli kihistoria amekubali sera ya kuunga mkono "serikali ya siku hiyo" ili kuhakikisha utulivu wa viwanda na ustawi wa wafanyakazi. Kwa kushirikiana na utawala wa sasa wa Rais William Ruto, anahakikisha ushawishi unaoendelea na kulinda nafasi yake licha ya kuwa upande wa Miungano wa AZIMIO katika kampeni zilizopita, baadaye aligeukia mlengo wa Kenya Kwanza.
Kwa nini Atwoli anamkosoa Uhuru Kenyatta?
Falsafa ya Atwoli inatokana na kudumisha uhusiano wa kikazi na serikali iliyopo madarakani, bila kujali ni nani, ili kuepuka kuvuruga uhusiano wake na vyama vya wafanyazi na kulinda mahusiano na waajiri.
Wakati wa enzi ya Uhuru Kenyatta, Atwoli alishirikiana na kumuunga mkono kwa vile alikuwa madarakani ambapo pia aliuunga mkono muungano wa AZIMIO COALITION uliasisiwa Hayati Raila Odinga kwa vile muungano ule 'handshake' ulipigiwa upatu na Uhuru akiwa Rais.
Kutokana na mabadiliko ya utawala mpya, Atwoli alihamishia ushirikiano wake kwa Rais Ruto, ambayo ni hatua iliyopangwa ili kuweka COTU karibu na serikali kuu ili kushawishi sera za kazi.
Ni kwa nini Atwoli anaubeza upinzani?
Wakati Atwoli anadai "hakuna upinzani kenya, kwa mtazamo hii ni kauli ya kisiasa inayolenga kuimarisha utulivu wa kisiasa hasa kutuliza joto la Kisiasa miongoni mwa vyama vya wafanyakazi. Matamshi yake hata hovyo yanamsuta kwa vile yeye mwenyewe alikuwa upinzani akishabikia muungano wa AZIMIO . Haimaanishi kwamba endapo yeye aligeukia upande wa Serikali hivo basi upinzani ulikufa. Kama alivyoshabikia Muungano wa AZIMIO na kwa jinsi Muungano huo ulivyoasisiwa na Hayati Raila Odinga hivyo hivyo Muungano mwingine unaweza kuzaliwa kutokana na milengo na vyama vya siasa vilivyopo.Hata hivyo tunaweza kusema kwamba Atwoli ni mweledi wa siasa za Kenya na kauli hizi zinazotoka kinywani mwake ni hatua ya kimkakati ya kujijengea taswira kama muungaji mkono wa serikali ya sasa ili kupata huruma 'sympathy' kwa utawala uliopo huku akiwabeza wapinzani na wakosoaji kisiasa wa serikali.
Bendera Fuata Upepo
Kutokana na historia yake ndefu ya kushirikiana na upande unaoshinda ili kudumisha udhibiti wa vuguvugu la wafanyakazi, Atwoli ana hulka ya Bendera Fuata Upepo. Ni mtu anayejua kusoma alama za nyakati akipita enzi za Moi, Kibaki, Uhuru, na sasa Ruto. Inasadikiwa kwamba hata kama uongozi wa sasa usiposhinda uchaguzi ujao wa mwaka 2027, Atwoli atahamia upande wa rais ajae ili kudumisha nafasi yake.
