#WINGU ZITO LIMEGHUBIKA KASHAFA YA PASSPORT ZA KENYA KWA WAGENI

Baada ya ukimya uliodumu kwa muda wa takriban wiki tatu, hatimaye Katibu katika Wizara ya Uhamiaji, Belio

Kipsang, Jumatatu Tarehe 16, Machi 2026, alitoa maelezo kwa ufupi sana alipokuwa akiongea mbele ya kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama taarifa iliyopeperushwa na Runinga ya Citizen Tv Kenya. 


Hata hivyo, maelezo yake yalikuwa mafupi mno kama tone la maji jangwani yakishindwa kukata kiu ya umma uliokuwa na shauku ya kupata ukweli au maelezo ya kina kuhusu sakata hilo, maelezo hayo yalizidi kutonesha kidonda cha maswali yasiyo na majibu.

Afisa huyo mwandamizi  hakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu taarifa zilizosambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Hakuweka bayana kama madai hayo ni ya kweli au la, wala hakukanusha moja kwa moja. Badala yake, alijikita kueleza tu vigezo vya msingi vya kupata pasipoti kuwa ni raia wa Kenya mwenye kitambulisho na cheti cha kuzaliwa maelezo ambayo kwa wengi yalionekana kuwa ya kawaida na yasiyogusa kiini cha sakata lenyewe.

Hata hivo haikubainika wazi iwapo alialikwa mbele ya kamati hiyo mahsusi kujibu uvumi huo au kama suala hilo lilijitokeza tu katikati ya mjadala wa mada nyingine. Hali hii imeacha maswali mengi yakining’inia hewani, mithili ya wingu zito lisiloonyesha dalili ya kunyesha lakini likitisha kwa uwepo wake. 

Kashfa ya nyaraka hizo za kusafiria za Kenya zilizodaiwa kutolewa kwa wageni iliibuliwa kwa mara ya kwanza kupitia  Mwanaharakati Boniface Mwangi kupitia nyaraka zilizovuja  kutoka idara ya Uhamiaji ya Kenya zilizohusiana na habari hiyo kupitia mitandao wa ' Citizens Rights in Africa Initiative' Miongoni mwa majina yaliyokuwemo kwenye orodha hiyo ni pamaoja na:-

1. Wicknel Chivayo, Mfanyabiashara wa Zimbabwe 

2.Alqoni Hamdan Dagalo Musa (Nduguye Mohammed Hamdan Dagalo)

3. Shareif Mohammed Osman.

4. Taha Osman Ishag Adam.

5.Siddiq Elsadig Elsiddig Elmahdi.

6. Omar Bashir Mohamed Manis.

7. Samy Ahmed.

8. Mayada Hamdan.

Ilikuwa ni matarajio ya wakenya  kwamba baada ya kimya hicho kirefu, ilikuwa ni fursa kwa idara ya uhamiaji kutoa majibu ya kina: Je, nyaraka hizi nyeti zilitolewa kwa wasiokuwa raia? Je, kuna uchunguzi unaoendelea? Na kama ndio, wananchi wanapaswa kusubiri kwa muda gani kabla ya kupata majibu ya mwisho? Lakini majibu hayo bado hayajapatikana.

Kama methali isemavyo, 'kidonda hakifichiki na kama wanavyosema wanataarabu, 'pembe la ng’ombe halifichiki kwenye pakacha' ukweli una njia yake ya kujidhihirisha. Hili linaonekana kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka; haijulikani ni lini au wapi, lakini ni dhahiri kuwa wakati wake utafika.

Kuibuka kwa kashfa hiyo kulihusishwa kwa namna moja au nyingine na  matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na Naibu  Rais wa zamani  wa kenya aliyetimuliwa, Rigathi Gachagua kuhusu mahusiano ya kundi hilo na Ikulu ya Nairobi. 

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, Rigathi Gachagua, amekuwa akitoa madai mazito kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii yanayowahusisha baadhi ya watu waliotajwa kupewa hati za kusafiria za Kenya kinyume Cha Sheria wakiwemo Waasi wa Sudan wenye kundi la Rapid Support Forces, RSF.

Tarehe 24 Julai 2025, Akiwa kwenye runinga ya KTN, Rigathi alidai kuwepo kwa uhusiano wa kibiashara kati ya serikali na kundi la waasi wa Sudan la RSF, linaloongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo, Katika sakata la passport lililovuja, mtu anayedakiwa kuwa mdogo wake ni miongoni mwa waliotajwa.

Gachagua Alidai pia kwamba mnamo mwaka 2023, aliagizwa kumwalika kiongozi huyo kwa mazungumzo ya kibiashara na Rais  wa Kenya alipokuwa bado madarakani.

Kati ya tarehe 7–10 Agosti 2025 akiwa ziarani Marekani, alitoa madai mengine mazito akihusisha uongozi wa juu  wa serikali ya Kenya na makundi hatari kigaidi ya somalia, jambo lililozua taharuki kubwa ya kisiasa.

Kauli hizi zilipingwa vikali na viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, pamoja na Naibu wa Rais Kithure Kindiki, waliomtaka Gachagua afike mbele ya vyombo vya uchunguzi baada ya kurejea kutoka and. Hata hivyo, haijulikani wazi hatua zilizochukuliwa baadaye. Kauli kama hizi zinapokosa majibu ya kina, huacha taswira ya mkanganyiko kwa wananchi. Wengine huanza kujiuliza: je, kuna ukweli uliofichika nyuma ya pazia la siasa? Kutokana na mazingira haya, ndio maana kilikuwa umuhimu mkubwa kwa Serikali kutoka ufafanuzi kwa Umma kusafisha upepo na kuondoa minong'ono.

Hofu kubwa inayowakumba wananchi si maneno ya viongozi pekee, bali uwezekano wa wageni kupata nyaraka halali za kitaifa. Hii ni hatari kwa usalama wa taifa, kwani inaweza kufungua mlango kwa uhalifu wa kimataifa, ugaidi, na hata kuchafua taswira ya taifa kwa mataifa mengine.

Na Kama hiyo haitoshi mnamo Tarehe 19 Februari 2026, Waziri wa mambo ya ndani Kipchumba Murkomen akiwa Nanyuki alidai kwamba  mabomu ya kutoa machozi yanamilikiwa na raia. kauli iliyowaacha wengi vinywa wazi.

Sasa unapoangalia kwa undani mlolongo wa matukio haya unaweza kupata taswira fulani, kwa mfano, Tarehe 5 Februari 2025  Rais William Ruto alitangaza kuondolewa kwa utaratibu wa upekuzi maalum ( Mandatory ID vetting) kwa wakazi wa kaskazini mwa Kenya wakati wa kupata vitambulisho vya kitaifa, akilenga kuondoa kile kilichoonekana kama ubaguzi.

Ingawa hatua hiyo ilisifiwa kwa kuleta usawa wa haki za kijamii, ilizua mjadala mpya kuhusu usalama wa taifa, hasa katika maeneo ya mpakani kama Wajir, Mandera, na Isiolo ambako kumekuwa na changamoto za kiusalama.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2023 hadi sasa, ukanda wa kaskazini mwa Kenya—hasa kaunti za Wajir, Mandera na Isiolo—umekuwa ukikumbwa na msururu wa matukio ya kiuhalifu yanayohusisha ujambazi, mauaji, na wizi wa mifugo. Matukio haya, yanayotokea mara kwa mara, yameendelea kuchora taswira ya eneo lililozongwa na changamoto za kiusalama, huku wananchi wakiendelea kuishi kwa hofu na sintofahamu. 

Baadhi ya matukio yaliyoropotiwa ni kama haya:-

Mnamo tarehe 12 Januari 2023, katika kaunti ya Wajir, watu wasiojulikana wenye silaha walivamia kijiji kimoja na kuwaua wachungaji wawili waliokuwa wakilisha mifugo yao, huku wakitoroka na kundi kubwa la ngamia. Tukio hili lilizua taharuki kubwa, hasa kutokana na mbinu zilizotumika ambazo zilionekana kuwa za kitaalamu.

Baadaye, tarehe 3 Machi 2023, katika kaunti ya Mandera, shambulio la kuvizia liliripotiwa ambapo basi la abiria lilishambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo. Watu kadhaa walijeruhiwa vibaya, na mali kuporwa, hali iliyosababisha kusimamishwa kwa safari katika barabara hiyo kwa muda.

Katika kaunti ya Isiolo, tarehe 18 Juni 2023, mapigano ya kikabila yalizuka kati ya jamii mbili jirani, yakihusisha wizi wa ng’ombe zaidi ya 200. Katika tukio hilo, wachungaji watatu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku familia zikilazimika kuhama makazi yao kwa hofu ya kulipiziwa kisasi.

Mwaka 2024 nao haukuwa tofauti. Tarehe 9 Februari 2024, County ya Mandera, kundi la majambazi lilivamia boma moja usiku na kuua mfugaji mmoja kabla ya kuondoka na mbuzi na kondoo zaidi ya 150. Tukio hili liliripotiwa kuwa sehemu ya mlolongo wa mashambulizi ya aina hiyo katika eneo hilo.

Mnamo tarehe 27 Aprili 2024, County ya Wajir ilishuhudia tukio jingine la kusikitisha ambapo wachungaji wawili waliuawa katika uvamizi wa asubuhi na mapema, huku wavamizi wakichukua ng’ombe kadhaa. Wanakijiji walilalamikia kuchelewa kwa vyombo vya usalama kufika eneo la tukio.

Katika County ya Isiolo, tarehe 14 Agosti 2024, kundi la watu wenye silaha lilivamia msafara wa wafanyabiashara, likiwapora fedha na bidhaa, na kumuua dereva mmoja papo hapo. Tukio hili liliongeza hofu miongoni mwa wafanyabiashara wanaotegemea barabara hiyo kwa shughuli zao za kila siku.KASHFA YA PASSPORT

Mwaka 2025 uliendelea kushuhudia hali hiyo. Tarehe 6 Januari 2025, katika County  ya Mandera, wachungaji wanne waliuawa katika shambulio lililohusisha wizi wa mifugo, ambapo zaidi ya ng’ombe 300 walichukuliwa na washambuliaji. Tukio hili lilielezwa kuwa moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya wizi wa mifugo katika eneo hilo.

Baadaye, tarehe 21 Mei 2025, katika County  ya Wajir, kuliripotiwa tukio la utekaji nyara wa mfanyabiashara mmoja maarufu, ambaye aliachiliwa baada ya siku kadhaa, hali iliyozua maswali kuhusu mtandao wa uhalifu unaoendelea kuota mizizi katika eneo hilo.

Katika County ya Isiolo, tarehe 2 Oktoba 2025, mapigano ya kulipiza kisasi yalizuka kufuatia wizi wa mifugo, ambapo watu watatu waliuawa na makumi ya familia kuhama makazi yao.

Hata mwaka 2026 haujaanza vyema. Tarehe 11 Januari 2026, County  ya Wajir, shambulio jingine liliripotiwa ambapo watu wawili waliuawa na mifugo kuibwa, huku washambuliaji wakitoroka bila kukamatwa.

Matukio haya, yanayojirudia kama mkondo wa maji usiokoma, yanaonyesha wazi kuwa changamoto za kiusalama katika ukanda huu bado ni kubwa. Wizi wa mifugo, ambao zamani ulionekana kama migogoro ya kijadi, sasa umechukua sura mpya ya uhalifu unaopangwa kwa ustadi unaohusisha silaha za kisasa na mbinu za hali ya juu.

Kwa mtazamo mpana, hali hii ni kama jeraha linaloendelea kuvuja damu bila kupatiwa tiba stahiki. Wananchi wanaendelea kuishi kwa hofu, huku wakisubiri hatua madhubuti kutoka kwa mamlaka husika. Kwa sababu kama wahenga walivyosema, penye moshi pana moto, eneo la kaskazini mwa Kenya, moshi huu unaonekana kuongezeka kila uchao.

Makala hii ya uchambuzi imeandaliwa kutoka kwenye mkusanyiko wa vyanzo mbalimbali.

Tupatie maoni yako.


Post a Comment

Previous Post Next Post