#VIONGOZI WA KISIASA WASALITI FAMILIA ZA WANA GENZ KWENYE MAANDAMANO YA JUNI 25


Maandamano ya kumbukumbu ya vijana wa
Gen Z yaliyofanyika nchini Kenya leo, Juni 25, yameacha maswali mengi miongoni mwa wananchi baada ya baadhi ya viongozi wa kisiasa walioonekana mstari wa mbele katika shughuli hiyo kuwasaliti wanafamilia za wahanga wa ukatili wa polisi wa Juni 25, 2024. Wazazi na wanafamilia wa waathirika hao wameonekana kama yatima baada ya viongozi hao wa kisiasa kuwatelekeza na kukimbilia kwenye magari yao baada hali kuwa tete walipokaribia majengo ya Bunge yenye ulinzi wa askari polisi waliojihami kwa silaha na magari ya kukabiliana na ghasia.

Miongoni mwa viongozi hao walionaswa kwenye kamera wakijinasua kutoka kwenye maandamano hayo na kuingia kwenye magari yao ni Jaji msitaafu David Maraga na baadaye Martha Karua, Kalonzo Musyoka nam Eugene Wamalwa.

Hata hivyo viongozi wa wanaharakati na watetezi wa haki za Binadamu na mkuu wa shirika la Vocal Africa Khalid Hussein wameonekana kusimama na familia hizo hado kwenye uzio wa majengo ya Bunge ambapo walitumia muda mchache kuweka mashada ya maua na kufanya maombi.

Viongozi mbalimbali wa upinzani na wanaharakati, akiwemo Martha Karua, James Orengo, Eugene Wamalwa, David Maraga na Kalonzo Musyoka, walishiriki maandamano hayo yaliyolenga kuwakumbuka vijana waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya mwaka 2024.

Hata hivyo, baada ya shughuli hiyo kumalizika na hali ya taharuki kuanza kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo, lawama zimeanza kuelekezwa kwa viongozi hao baada ya kuonekana wakiondoka kwa magari yao huku wazazi na ndugu wa wahanga wakibaki nyuma wakikabiliana na mazingira magumu ya usafiri na usalama.

Kwa mujibu wa baadhi ya washiriki wa maandamano hayo, wazazi wa wahanga walikuwa wamejitokeza kwa matumaini kwamba viongozi waliokuwa wakizungumza kwa niaba yao wangeendelea kuwa karibu nao hadi mwisho wa shughuli hiyo. Badala yake, wengi walidai kuhisi kutelekezwa wakati viongozi walipoondoka eneo la maandamano.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema tukio hilo linaibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya viongozi wa kisiasa katika harakati za kijamii. Je, ushiriki wao ni wa dhati katika kutafuta haki kwa waathirika na familia zao, au ni njia ya kujijengea mtaji wa kisiasa kupitia maumivu ya wananchi?

Kwa upande mwingine, kumekuwepo na taarifa kwamba kuondoka kwa viongozi hao wa kisiasa katika maeneo yake kunatokana na sababu za kiusalama ambapo inadaiwa baadhi Yao huenda wangekamatwa na maafisa wa polisi kwa madai ya uchochezi.   Hata hivyo, hoja hiyo haijawanyamazisha wakosoaji wanaodai kuwa viongozi hao walipaswa kuhakikisha wazazi na familia za wahanga wanapata msaada na ulinzi wa kutosha kabla ya kuondoka.

Kile ambacho hakiwezi kupingwa ni kwamba familia za vijana waliopoteza maisha bado zinaendelea kubeba mzigo mzito wa majonzi, maumivu na maswali yasiyo na majibu. Wanachohitaji zaidi ni haki, ukweli na mshikamano wa kweli, si hotuba za kisiasa pekee.

Kadri mjadala huu unavyoendelea, wananchi wengi wanasubiri kuona kama viongozi waliokuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo watajitokeza kueleza kilichotokea na hatua walizochukua kuhakikisha usalama wa wazazi na wanafamilia wa wahanga waliokuwa wameandamana pamoja nao.

Je, hili ni tukio la kawaida lililosababishwa na changamoto za usalama, au ni ishara ya viongozi kutumia maumivu ya wananchi kwa maslahi ya kisiasa? Huo ndio mjadala unaoendelea kutawala nchini Kenya baada ya maandamano ya kumbukumbu ya Gen Z ya Juni 25.

Post a Comment

Previous Post Next Post