Ni Kenya tu ambapo ulinzi wa Rais wa Nchi unaweza kuwa mchezo wa sandakarawe, ambapo mtu yeyote anayejisikia anaweza kujitosa
kwenye jukwaa la Rais kwenye mkutano wa hadhara na kuzua tafrani. Jambo linalokereketa na kuzua maswali ni kwanini Matukio yamekuwa yakijirudia mara kwa mara?Ukiangalia mlolongo wa visa vilivyojitokeza awali huwezi kuondoa hofu ya kuwepo njama miongoni mwa Kikosi cha Ulinzi Cha msafara wa Rais aidha kumdhalilisha au kumdhuru. Tunadhani ni haki ya wakenya kujua nini kilichojiri au sababu gani hasa zilizopelekea kuhatarisha usalama wa kiongozi wa Nchi. Nini walichokikosa walinzi wa Rais? Walipungukiwa nini? Walikuwa wapi? Au ni kufanya kazi kwa mazoea?
Hatua ya inspector Generali wa Polisi kuunda tume ya kuchunguza matukio haya imekuja kwa kuchelewa sana. Kwa Nchi zilizoendelea maafisa husika muda huu walipaswa kuwa korokoroni pindi uchunguzi ulifanyika.
Kama taifa linaweza kushuhudia visa zaidi ya kumi vinavyohatarisha ulinzi wa Rais, haitoshi Generali Kanja kuona Umuhimu leo na isiwe Jana au juzi. Kwa maana nyingine hata yeye ndo anagutuka sasa kutoka usingizini.
Ni matarajio ya wakenya kwamba baada ya mabadiliko yaliyofanywa kwenye kikosi Cha ulinzi kwenye msafara wa Rais jambo hili halitajirudia tena. Aidha ni matumaini ya wakenya kwamba ukweli utabainishwa na pale ambao uzembe umefanyika hatua za kinidhamu/Kisheria zichukuliwe kwa Wahusika.
