Miongoni mwa Majanga makubwa yanayoikabiri Dunia kwa sasa na tangu Miongo kadhaa iliyopita ni Janga la Ukimwi. Athari za Janga hili zimekuwa maradufu katika
nchi za ulimwengu wa tatu kusini mwa Jangwa la Sahara. Maelfu ya watu wameangamia kutokana na Janga hili tangu Miaka ya Themanini (1980's) ulipogundulika ugonjwa huo kwa mara ya kwanza.Imekuwa ni hulka ya Binadamu kuwa Maradhi ni siri ya mtu hadi pale anaposhindwa kuyadhibiti inakuwa sio siri tena. Kwa wale wenye kumbukumbu mnaweza kukumbuka kilichotokea Tanzania mwaka 2006 pale alipojitokeza Babu wa Loliondo, Ambikile Mwasapile Kule Samunge, na tiba ya kikombe Cha babu ambapo maelfu walimiminika kutoka Africa mashariki bila kujali ni nani na alitoka wapi, kwenye msafara wa mamba na kenge walikuwamo, hata wale ambao hawakudhaniwa kuwa na uhitaji wa kikombe Cha Babu nao walikuwapo.
Samunge iligonga vichwa vya habari kutokana na Tiba ya kikombe Cha babu ambacho kwa Imani pia kilikuwa na uwezo wa kutibu ukimwi. Kuna walioshawishika kuacha dozi ya Dawa zao ilimradi tu wamekunywa kikombe Cha babu.
Ilikuwa ni patashika na hekaheka Kule Samunge ikiwemo watu kukwama njiani wakiwa safarini kuelekea huko, si helikopita, magari binafsi au mabasi yalielekea huko, lakini hata walipofika huko foleni ili kupata kikombe Cha Babu ilihitaji uvumilivu mkubwa. Lakini yote tisa, kumi ni kwamba watu wako kimya ila Wana majeraha mioyoni mwao kutokana na pigo la Janga la Ukimwi.
Tarehe 26, Feb 2026, Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale alizindua chanjo mpya ya Ugonjwa wa Ukimwi pale Riruta Health Centre, kwa Jina la Lenacapavir ( Trade name :Sunlenca) Hatua hii ilipokelewa kama Nuru iliyowaka gizani au tumaini jipya lililokawia katika kipindi hiking ambapo wagonjwa wa Ukimwi wanaishi kwa kutumika Dawa za kila uchao.
Katika makala hii tunapiga darubini kwenye mambo machache kuhusiana na uzinduzi wa chanjo hii.
1.CHANZO CHA UZALISHAJI
Chanjo hii imetengenezwa na Kampuni ya Glead Sciences yenye makao yake Jimbo la California nchini Marekani. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) liliidhinisha chanjo hiyo mnamo Mwezi July mwaka 2025. Aidha Taasisi ya vyakula na Dawa ya Kenya iliidhinisha chanjo hiyo mnamo Mwezi Januari mwaka 2026.
2. USAMBAZAJI
Chanjo hiyo inasambazwa na Serikali ya Kenya chini ya Wizara ya afya kwa ushirikiano na Shirika la Global Fund na Kampuni ya Glead Sciences. Serikali ya Kenya imetangaza kuanza kutoka chanjo hiyo kwenye Wilaya (Counties) 15 za mwanzo kama Majaribio
3. MATUMIZI
Kwa mujibu wa maelekezo ya Wizara ya afya ya Kenya, chanjo hiyo inatumika kwa dozi ya mara mbili kwa mwaka kila baada ya miezi Sita.
4. GHARAMA
Gharama ya chanjo hiyo inakadiriwa kuwa Shilingi za Kenya kati ya Alfu 6-7 kwa awamu moja ya Matibabu.
5.WALENGWA
Wenye sifa za kupata chanjo hiyo ni wale wasiokuwa na maambukizi ya Ukimwi japo ambao hata hivyo wapo kwenye hatari ya kuambukizwa.
HOJA MUHIMU
1. Serikali haijatoa taarifa kwa Umma kuhusiana na Gharama za jumla za uwezeshaji wa utoaji wa chanjo hiyo, kuhusu uwepo uwezekano kama ni Ruzuku au msaada, au ni kwa gharama gani lengo litafikiwa.
2. MAJARIBIO
Kwa nini chanjo hiyo itolewe kwa majaribio nchini Kenya kwa mantiki kwamba Kule inakotoka ilishajaribiwa kiwango Cha ubora wake, vinginevyo isingetolewa au kuruhusiwa kusambazwa. Unapofanya Majaribio kuhusu jambo au kitu Fulani maana yake kuna matokeo hasi au chanya. Kwa maana nyingine wakenya watarajie majibu ya majario ya chanjo hiyo ambayo tayari imeshaidhinishwa kutumika.
Je, tutarajie matokeo ambayo huenda yakawa na athari zaidi au tofauti na Yale yaliyofanywa mzalishaji wa kwanza?
3.USAMBAZAJI
Serikali haijaeweka bayana kwamba lengo la kuanza na hizo County 15 ni kutokana na kungojea majibu ya majaribio ili baadaye zisambazwe kote nchini? Ni uchache wa chanjo hizo au vinginevyo?
4.UHAKIKA WA UPATIKANAJI ENDELEVU
Kwa kuwa matumizi ya chanjo hiyo Bado yanaonekana kutokuwa na ukomo, Serikali imejiridhisha kwa kiasi gani kuhusu uhakika wa upatikanaji wa chanjo? Aidha haijaeweka Waz
i mpango madhubuti wa muda mrefu kuhakikisha chanjo hiyo inapatikana kipindi chote kwa walengwa.
5.GHARAMA ZA UAGIZAJI
Serikali haijaeweka bayana kuhusiana na gharama za uagizaji na usambazaji wa chanjo hiyo. Mantiki ya hoja hii imejengeka katika msingi kwamba endapo uagizaji unategemea Ruzuku au Wafadhili, itakuwaje au nini kitachofanyika pale watakapojiondoa katika usaidizi wa aina hiyo? Mathalani itakumbukwa madhara ambayo hadi sasa yanang'ata machungu yake baada ya Rais wa sasa wa Marekani kujiondoa katika mikataba mingi ya kimataifa ikiwemo Ile ya USAID ambayo ililemaza idara na vitengo mbalimbali vya afya.Na je, endapo Serikali inaagiza chanjo hiyo kwa fedha zake yenyewe, je imetengwa bajeti endelevu?
6.HAMASISHO LA UKOMO WA MATUMIZ
Je, serikali imeuhamasisha Umma kwa kiasi gani hasa kuhusiana na uwezekano wa watu wengi kukimbilia kuanza kuitumia chanjo hiyo na kisha kuacha. Kuna mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuwekwa wazi kwa Wananchi ili wajue kwa mfano inasemekana kwamba kuanza kuitumia chanjo hiyo na kisha kuacha kunaweza kuwa na matokeo hasi na yenye madhara hata kuliko mtu ambaye hajaitumia kabisa.
7. ATHARI ZA KIUCHUMI
Katika mtazamo mwingine inaonekana ujio wa chanjo hii utaongeza changamoto za kiuchumi kwenye jamii. Hapa linaongezeka kundi lingine la watu ambao kimsingi hawaugui Ukimwi lakini na wao pia watahitaji kuwa matibabu ya kuchomwa hiyo sindano ya chanjo mara mbili kwa mwaka bila ukomo.
Kama hiyo haitoshi itakuwa vigumu kwa watu wenye dalaja la chini kimaisha kumudu gharama za chanjo hiyo hasa ikizingatiwa hali ilivyo ya ugumu wa maisha kiasi Cha kupata hata mlo wa siku, hiyo pesa ya kulipia chanjo unaitoa wapi? Kwa walio wengi hili litasalia kwa wenye pesa zao walala hoi tutasikilizia redioni.
8. RUSHWA NA UKIRITIMBA WA WAHUDUMU WA AFYA
Kutokana na ukweli kwamba chanjo hii ni mpya na ndo kwanza inaingia nchini, huenda kukawa na uhitaji mkubwa kuliko dozi zilizopo. Matokeo yake WAHUDUMU WA AFYA wanawrza kupandisha bei au gharama husika ili kujinufaisha.
Lakini pia si jambo geni ukaambiwa chanjo imekwisha ilihali ingalipo ili mradi tu kutengeneza mianya ya rushwa na kwa vile County zilizoorodheshwa kupokea chanjo hizo ni chache kuliko zilizosalia kuna uwezekano wa watu kusafiri kutoka County moja kwenda nyingine ili kupata huduma hiyo. Matokeo yake ni kwamba kutakuwa na upungufu mkubwa.
Yote tisa, lakini kumi ni matumaini yetu kwamba ujio wa chanjo hii utakuwa hatua muhimu katika mapambano dhidi ya Janga la Ukimwi. Tunatarajia kuona serikali ikionyesha jitihada zaidi kuhakikisha upatikanaji wa chanjo hii kwa wote pindi tunasubiria kuona athari za ufanisi wake.
Ushari nasaha: Ukipata chanjo hiyo usijiachie maana hujayajua ya mbeleni
