# JE, KAULI YA NCHIMBI NI DHAHIRI?

 Kauli ya Makamu wa Rais wa Tanzania Nchimbi — Uchambuzi wa KinaKauli ya Nchimbi Ina mashiko?

Utangulizi: Saa ya Ukweli Imewadia

Siku ya 24 Julai 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, katika Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, alitoa kauli ambayo imezunguka mitandaoni kama umeme wa radi — kauli hii ya Nchimbi imejadiliwa kwa mapana na marefu kwenye majukwaa mbalimbali ya kijamii bila jibu mwafaka, nini hasa kilichomo ndani ya kauli hiyo.

Mtu mwenye wadhifa wa makamu wa Rais huwa na hofu ya "kuukwaa Urais" Wazungu husema, He suffers the heartbeats of presidence." Na kweli, mtu anayeketi katika kiti cha pili kwa itifaki ya Taifa, ambaye amezoea kuisikia harufu ya ikulu Kila macheo na machweo, sasa amepaza sauti. Siyo sauti ya kawaida. Ni sauti inayobubujika kama chemchemi ndani ya jangwa la haki iliyopotea. Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika Mkutano Mkuu wa THRDC tarehe 24 Julai 2026, alisema maneno yasiyo ya kawaida kwa mtu aliyeketi kwenye kiti cha enzi cha serikali: "....Wananchi waipiganie katiba mpya....."  ​

Haya si maneno ya mtu wa kawaida. Haya ni maneno ya mtu anayeinusa harufu ya Urais, anayesikia mapigo ya moyo yakimwendea Kasi kwa kukikaribia kiti cha enzi, akisema kwa sauti ya dhahiri: "Kusanyeni nguvu zenu, mziweke katika msingi wa kuipigania Katiba mpya katiba mpya."  Lakini swali ni hili: Je, hii ni chemchemi ya kweli au ni mtego wa fisi mwenye njaa?

Uchambuzi wa kina:

Sehemu ya Kwanza: 

 Mukhutadha wa Nini Alichosema Nchimbi?

Kwa lugha nyepesi lakini yenye uzito wa chuma, Nchimbi alitoa mawazo makuu matatu:

Kwanza: "Katiba ndiyo sheria kuu ya nchi yenye mamlaka ya kubatilisha au kufuta sheria yoyote inayokinzana nayo mara tu inapopitishwa."  Hapa anaweka msingi — kwamba katiba ndiyo mawe ya msingi ya nyumba yote. Bila msingi imara, nyumba yote itaporomoka.

Pili: "Badala ya kutawanya nguvu za kisiasa kwenye masuala madogo madogo, wananchi wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kupigania Katiba Mpya."  Hapa anawataka watanzania wasitawanye mizinga, bali waelekeze risasi zote katika lengo moja — katiba.

Tatu: "Hakuna mashindano ya nani anaanza. Haki ni msingi wa amani. Haiwezekani mtetezi wa amani akawa adui wa haki."  Hapa analenga kupiga mstari kati ya haki na amani, akisema kwamba haki na amani ni pacha — hawawezi kutenganishwa. ​

Lakini, ndugu msomaji, hebu tukae chini tufikirie: Je, kauli ya Nchimbi ulitoka moyoni, au ni kauli iliyopangwa kama mchezo wa karata?

Sehemu ya Pili: 

JE, huu ni Mtego au Vuguvugu jipya ndani ya Serikali ya Samia?

1. "He Suffers the Heartbeats of Presidence" — Dhamira ya Urais

Emmanuel Nchimbi anainusa harufu ya Urais.  Anajua kwamba katika mazingira yoyote, ikiwa kitu kitatokea kwa Rais Samia Suluhu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti hicho. Kwa hiyo, kwa nini mtu ambaye ana nafasi kubwa ya kuwa Rais wa 7 wa Tanzania angetoa kauli inayopingana na mwelekeo wa serikali yake?

Hapa kuna njia mbili za kufikiria:

Njia ya Kwanza (Mtego):

 Nchimbi anajua kwamba wananchi wanataka katiba mpya. Anajua kwamba shinikizo la wananchi linazidi. Anajua kwamba kama atakaa kimya, wananchi watamwona kama sehemu ya tatizo. Kwa hiyo anatoa kauli nyepesi — "waipiganie katiba" — lakini bila kutoa njia ya kufanikisha azma hiyo.... hivyo, Ni kama mtu anayemwambia mnyonge "pigania haki yako"  huku akijua kwamba mnyonge huyo hana silaha, hana jeuri, hana hata uwezo wa kupiga kelele. Ni kauli ya kumfariji, si ya kumkomboa.

Njia ya Pili ni mwanzo wa Vuguvugu ndani ya Serikali:

 Nchimbi anajua kwamba katiba ya sasa inampa Rais mamlaka makubwa mno. Anajua kwamba hata yeye mwenyewe, ikiwa atakuwa Rais, atataka mabadiliko. Kwa hiyo anasema ukweli — kwamba katiba mpya ndiyo njia pekee. Anawaambia wananchi "piganieni"  kwa sababu anajua kwamba bila shinikizo la wananchi, hakuna kitu kitatokea.

Lakini swali la msingi ni hili: Je, Nchimbi ameonyesha jitihafa zozote za kufungua milango ya mchakato wa katiba mpya ndani ya serikali? Je, amewasiliana na Rais kuhusu suala hili? Nini anachomshauri Rais kama Makamu wake? Je, ameunda kikosi kazi kwa ajili ya swala hiki? Je, ametoa muda, fedha, au rasilimali yoyote? Kama jibu ni "hapana,"  basi kauli yake ni kama debe tupu haina mashiko kwa Wananchi wenye kiu ya kupata katiba mpya.

2. Samia Suluhu vs. Nchimbi: Je, Kuna Tofauti ya Kweli?

 Je, kauli hii inamaanisha kwamba Nchimbi anatofautiana na Samia? Hebu tuchambue kidogo:

Samia Suluhu amekuwa Rais tangu 2021. Katika kipindi hiki, amefanya mabadiliko kiduchu, amekuwa akiruhusu mikutano ya siasa /hadhara kwa jinsi anavyojisikia mwenyewe, amelegeza uhuru wa vyombo vya habari kidogo sana, amewaachia wafungwa wa kisiasa kadhaa. Lakini kuhusu katiba mpya, amekuwa kimya kama mizimu ya usiku. Licha ya kulisema Hilo kwenye mpango wake, hakuna dalili za utekelezaji wake. Ni kama mbinu ya kuuziba mwanya wa maswali ili ionekane ana mpango na swala la katiba mpya.

Nchimbi, kwa upande wake, amesema moja kwa moja: "Waipiganie katiba"  Hii ni tofauti kubwa. Samia anasema "subirini"  — Nchimbi anasema "piganieni."  Samia anasema "muda utaamua"  — Nchimbi anasema "nguvu zenu zielekezeni huko." 

Lakini hebu tuulize: Je, Nchimbi alisema haya kwa ruhusa ya Samia? Au alisema kwa ajili yake mwenyewe? Ikiwa alisema kwa ruhusa ya Samia, basi hii ni mchezo wa karata — Rais anang'ata, makamu wake anapulizia kidonda. Ikiwa alisema bila ruhusa, basi hii ni tofauti ya kweli, na inaweza kuwa mwanzo wa mapambano ndani ya Ikulu.

3. "Kuipigania katiba maana yake nini?"  Nini Maana Yake Katika Nchi ya inaongozwa kwa mkono wa Chuma? Na Rais ambaye kwake Uanaharakati ni ugaidi?"Kuipigania maana yake ni kwamba ni jambo ambalo linapingwa na serikali!"Ni jambo ambapo linahitaji uanaharakati wa ukombozi, Na hapo ndipo utata ulipo.

Nchimbi anasema "waipiganie katiba mpya."  Lakini katika nchi ambayo:

Rais ni 'MUNGU MTU'

 Mikutano ya siasa inapigwa marufuku kwa utashi wa Rais 

 Uhuru wa maoni ni kosa la uhaini

 Ukosoaji wa serikali unagharimu  kifungo

 Maandamano ya Raia ni kosa la jinai 

Je, watanzania wataipiganiaje katiba? Je, Nchimbi anawapa ruhusa ya kufanya mikutano? Je, anawapa ulinzi wa polisi? Je, anawasemea kwamba "fanyeni mikutano, mimi nitawalinda?"  Hapana. Anasema tu "piganieni"  — lakini bila kutoa mwelekeo, bila kufungua mlango, bila hata kuonyesha njia au nini ambacho yeye amekifanya ili iwe mfano wa kupigwa!?

Ni kama mtu anayemwambia mvuvi "Kalete samaki"  huku akijua kwamba mvuvi huyo hana mtumbwi, hana nyavu za kuvulia na bahari imefungwa, Ni kauli ya unafiki — unasema ukweli, lakini bila kutaka ukweli uweze kutekelezwa.

Sehemu ya Tatu: Hatua za Makusudi — Je, Zipo?

"Ni hatua gani za makusudi zilizochukuliwa na Samia Suluhu na makamu wake kudhihirisha nia ya kupatikana katiba mpya?" 

Jibu ni gumu: Tuchambue:

Samia Suluhu:

Je, alipeleka mapendekezo kutengwa kwa bajeti kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya? Hapana.

Ameunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba? Hapana.

 Amepeleka mswada wa katiba mpya Bungeni? Hapana.

 Ameruhusu mihadhara kujadili katiba mpya? Hapana.

 Ameondoa vikwazo vya mikutano ya siasa? Hapana.

 Ameongeza uhuru wa vyombo vya habari kuhusu Uhuru wa maoni? Hapana.

Emmanuel Nchimbi:

 Amemshauri Rais kuhusu umuhimu wa swala hili? Haijulikani.

Je, amefungua dawati la maoni kushughulikia katiba mpya? Hapana.

 Amepeleka barua ya rasmi kwa Rais kuhusu suala hili? Haijulikani.

 Amefanya mikutano ya kisiasa kujadili katiba? Hapana (mikutano imepigwa marufuku).

 Amehamasisha kutengwa kwa bajeti kwa ajili ya swala hili? Hapana 

Kwa hiyo, ndugu msomaji, hatua za makusudi ni sifuri kwa wote. Ni kama mtu anayesema "tujenge nyumba"  lakini hana mchanga, hana mawe, hana hata ramani. Ni maneno tu — maneno mazuri, lakini bila mifupa.

Sehemu ya Nne: Mtego wa Kisiasa — Je, Nchimbi Anawaficha Nini Watanzania?

Hapa ndipo mafumbo ya kauli hii yanapoanza kufichuka. Tufikirie hali hii:

Nchimbi anajua kwamba wananchi wanataka katiba mpya. Anajua kwamba shinikizo linazidi. Anajua kwamba ikiwa atakaa kimya, wananchi watamwona kama sehemu ya tatizo. Kwa hiyo anatoa kauli nyepesi — "waipiganie"  — ili:

1. Kujificha: Asionekane kama adui wa mabadiliko

2. Kuwafariji: Awapatie tumaini dogo ili wasiende kwenye njia kali zaidi

3. Kutoa muda: Awapatie "dawa ya pole pole" wakati serikali inaendelea kama kawaida

4. Kujipanga: Akijipanga vizuri kwa ajili ya Urais wake, aonekane kama "mwanamabadiliko"

Lakini kuna uwezekano mwingine: Nchimbi anajua kwamba katiba ya sasa inampa Rais mamlaka makubwa. Anajua kwamba hata yeye mwenyewe, ikiwa atakuwa Rais, atataka mabadiliko. Kwa hiyo anasema ukweli — kwamba katiba mpya ndiyo njia pekee.

Lakini swali ni hili: Kwa nini asiseme moja kwa moja? Kwa nini asiseme "Serikali itaanza mchakato wa katiba mpya mwezi wa Agosti 2026?"  Kwa nini asiseme "Nimeagiza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuundwa?"  Kwa nini anasema tu "waipiganie"  — maneno ya mtu anayekaa nje, si ya mtu anayekaa ndani?

Hapa ndipo unafiki ulipo. Ni kama mtu anayesema "tujenge daraja"  bila vitendea kazi. Anataka daraja lijengwe, lakini anataka wengine wajenge — yeye atakuwa mwanzoni wa kuvuka.

Sehemu ya Tano:

Endapo Nchimbi ana Nia ya dhati kwa kauli yake, je amejipangaje kukabiliana na mfumo dhalimu wa Boss wake? Kimsingi si Samia Suluhu anayepinga kuwepo katiba mpya, ila ni makundi ya walaji na wapigaji wenye maslahi na mfumo uliopo. Hapa Kuna makundi angalau manne: 

I)Ikulu: Kuna kundi la waandamizi wa Ikulu ambalo mabadiliko ya mfumo utakaoruhusu katiba mpya utawatema. Hivyo si watu wanaopenda mabadiliko kwa lengo la kutlkita mizizi ya unyonyaji kupitia mgongonwa Rais.

II) Kuna kundi la wanamtandao wa Jakaya Kikwete la tangu enzi ya 2005. Licha ya baadhi ya Wajumbe wake kufariki au kuzeeka, waliwakweza Watoto wao kwenye nyazifa muhimu ambao wanaendeleza sera zilezile. Kwa vile Kikwete Bado yupo na anaaminika kuwa mshauri Mkuu wa Samia Suluhu, Hawa ndio watu wasiotaka katiba mpya. Samia Suluhu anasadikiwa kuuenzi ushauri wa Kikwete kwa kila jambo kiasi kwamba baadhi wa wadadisi wanaamini Samia Suluhu ni Rais kivuli au Robbot inayoendeshwa na Kikwete. Kwa yeyote anayepinga hoja hii aeleze bayana  kwanini watu walioondolewa kwenye Serikali ya Mafuguli walirejeshwa na Samia Suluhu pindi tu baada ya kifo mtangulizi wake? Kama hiyo haitoshi aseme kwanini Samia Suluhu amekuwa akimtuma Rais msitaafu Kikwete kwenye ziara za kikazi za nje ya nchi huku kukiwepo na watu wengine lukuki ambao kimsingi wangeweza kumwakilisha.

Na zaidi ya yote atoe majibu kwanini mchakato wa Katiba mpya ulioanzishwa na Kikwete kipindi akiwa madarakani ulikwama? Nini kilichokosekana?

III) Kundi lililo Ndani ya CCM

Kuna kundi la watu ndani ya chama Tawala Cha CCM wanaoamini kwamba wao ndo wenye hati miliki ya Tanzania, na kwamba wengine waliosalia huenda ni wakimbizi kutoka nje, kundi hili linaamini kwamba mabadiliko yoyote lazima yaanzie ndani ya CCM, hawataki katiba mpya kwa Sababu utapunguza Nguvu za Chama Tawala kwenye Serikali.

IV) Ndani ya CCM Kuna kundi la Wakereketwa wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hili ni kundi linalojiapiza kuulinda muungano. Kundi hili linaamini kupatikana kwa katiba mpya ni tishio la Kuvunjika kwa muungano kwa Sababu kero nyingi za muungano zinaweza tu kutatuliwa na katiba mpya. Hatua hii inaweza kupelekea kuondolewa madarakani  Chama cha CCM katika upande wowote wa muungano aidha bara au visiwani. Hatua hiyo itahatarisha Kuvunjika kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao kwa sasa muhimili wake ni chama Cha CCM.

Je, Nchimbi anayajua haya? Bila shaka ANAJUA. Je anapotikisa kiberiti ana Nia ya kujua tu endapo zimo njiti ndani au Ganda tupu? ANAJUA matokeo yake? Je, yupo tayari kupambana? Au ni jaribio la kukaanga mbuyu awaachie wenye meno watafune?

Sehemu ya Sita: Methali, Nahau, na Mafumbo ya Kauli Hii

"Rais Anang'ata, Makamu Anapulizia Kidonda"

 Inamaanisha kwamba mtu mmoja analeta shida, mtu mwingine anajaribu kupunguza maumivu. Je, hii ndiyo hali ya Samia na Nchimbi? Samia anang'ata — anakataa katiba mpya, anawafunga wanaompinga, anawanyima uhuru. Nchimbi anapulizia — anasema maneno mazuri, anawafariji, anawapa tumaini dogo. Lakini kidonda bado kiko pale pale. Na kama kidonda kitaendelea kuvuja, hata upulizaji hautasaidia.

"Fisi Akilia Mchana, Mbwa Hafi Usiku"

Methali hii inamaanisha kwamba mtu anayetoa onyo mapema anafanya kazi nzuri. Nchimbi anatoa onyo — kwamba katiba mpya ni muhimu. Lakini je, ni onyo la kweli au ni wimbo wa fisi anayejificha? Fisi akilia mchana, mbwa hafi usiku — lakini kama fisi huyo ni mwenyeji wa boma, basi kilio chake ni cha unafiki.

"Mchimba Kaburi Huingia Mwenyewe"

Nchimbi anarusha mpira kwa Wananchi, "waipiganie katiba mpya" Yeye akiwa wapi? Je inamhusu? Lakini kama katiba mpya itapita, itapunguza mamlaka ya Rais ambapo yeye ni sehemu ya Urais...Itamfanya yeye, ikiwa atakuwa Rais, awe na mamlaka madogo zaidi. Kwa kwa maana nyingine anataka katiba itakayompunguzia mamlaka yake mwenyewe? Au anajua kwamba haitapita, na kwa hiyo anaweza kusema chochote bila wasiwasi?

Sehemu ya Saba: Nini Kilichojificha Ndani ya Kauli ya Nchimbi?

Kauli ya Nchimbi ina mafumbo matatu makubwa:

1.Fumbo la Kujipanga kwa Urais

Nchimbi anajua kwamba Samia Suluhu ana muda wake. Anajua kwamba siku moja, yeye atakuwa Rais. Anataka kuanza kujenga "brand" yake kama "mwanamabadiliko" mapema. Anataka watanzania wamwone kama mtu anayetaka mabadiliko, si kama mtu anayelinda status quo. Kwa hiyo anasema maneno mazuri sasa, ili baadaye apate ridhaa ya umma. Hata mambo yakikwama, apate pa kuanzia kwamba aliwahi kusema.

2. Mafumbo la Kuwafunga Wananchi Midomo

Kwa kusema "waipiganie,"  Nchimbi anawapa wananchi "dawa ya pole pole." Anawapa tumaini dogo ili wasiwe na mihemko ya Kisiasa  — kama vile kuandamana, kufanya mikutano ya hadhara, au hata kupiga kelele zaidi. Anawambia "piganieni"  — lakini kwa njia ya amani, kwa njia ya kufuata sheria, kwa njia ambayo haitaleta vurugu. Ni kauli ya kupunguza shinikizo, si ya kuongeza mabadiliko.

3. Mafumbo la Kujificha Mbele ya Historia

Nchimbi anajua kwamba historia itamwuliza: "Wewe ulikuwa wapi wakati watanzania walipokuwa wakipigania katiba mpya?"  Anataka kujibu: "Nilikuwa nikiwaambia waipiganie."  Anataka kuonekana kama alikuwa upande wa wananchi, si upande wa serikali. Anataka kuwa "mvua inayonyesha upande wa pili wa mlima" — anayetoa maji kwa wote, lakini bila kuchagua upande.

Sehemu ya Nane: Hitimisho — Ni muda wa ukweli na haki, Lakini Saa ya Kutenda Bado Inachelewa

Kauli ya Nchimbi ni kama maua mazuri yanayotolewa kwenye jeneza la mwendazake, yanavutia, lakini hayabadili ukweli kwamba ndani ya jeneza Kuna maiti. Ni kama sauti ya kengele inayolia mbali — inasikika, lakini haitoi msaada kwa mtu aliyeko kwenye hatari.

Lakini, ndugu msomaji, hebu tusije tukamkosea mtu. Naweza kuwa mwanzoni wa mabadiliko. Naweza kuwa mtu ambaye ameamua kusema ukweli licha ya hatari. Naweza kuwa "Moses" anayetangulia kabla ya "Joshua" wa kweli kufika.

Lakini hadi sasa, hatua zake zinaongea kwa sauti kubwa kuliko maneno yake. Na hatua zake zinasema: "Hapana." Hapana kwa mchakato. Hapana kwa mikutano. Hapana kwa uhuru. Hapana kwa katiba.

Kwa hiyo, kauli hii ni nini? Ni mtego kwa wananchi wa Tanzania. Ni njia ya kuwafariji kutoka kwenye mkono wa chuma. Ni unafiki wa aina fulani — unasema ukweli, lakini bila kutaka ukweli uweze kutekelezwa.

Lakini pia, ni chemchemi — chemchemi ambayo inaweza kuwa mwanzo wa mto. Mto ambao unaweza kuwa mwanzo wa bahari. Bahari ambayo inaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko.

Lakini mpaka sasa, ni chemchemi tu — ndogo, dhaifu, bila mto wake. Na kama hakutakuwa na mvua ya matendo, chemchemi hii itakauka kama mafuta ya asali jangwani.

Mwisho: Wimbo wa ukombozi,

Mwananchi wa Tanzania:

Mwananchi wa Tanzania anasikia maneno mazuri. Anasikia "waipiganie."  Lakini anajua kwamba mikono yake imefungwa. Anajua kwamba mdomo wake umezuiwa. Anajua kwamba hatua zake zitakabikiwa na risasi.

Kwa hiyo anauliza: "Nitaipiganiaje, baba? Nitaipiganiaje katika nchi ambayo kupiga kelele ni kosa? Nitaipiganiaje katika nchi ambayo kukusanyika ni uhaini? Nitaipiganiaje katika nchi ambayo hata waziri mkuu wa zamani aliyepigania katiba alifungwa? Nitaipiganiaje, baba, nikiwa sina silaha, sina jeuri, sina hata sauti?" 

Na Nchimbi anajibu: "Piganieni." 

Lakini mwananchi anauliza tena: "Nitaipiganiaje, baba, wakati wewe mwenyewe uliye na mamlaka ya kufungua mlango, unasimama nje ukisema 'piganieni' badala ya kufungua? Nitaipiganiaje, baba, wakati wewe unaweza kufanya kitu, lakini unachagua kusema tu?" 

Na upepo unajibu kwa kimya. Kimya kikubwa. Kimya cha jangwa. Kimya ambacho kinasema zaidi kuliko maneno yote.

Post a Comment

Previous Post Next Post